MPENZI NIKUPIKIE.
Embu leo kaa huko, maajabu ya nyangumi.
Leo niachie jiko, futari nipike mimi.
Nakupa mapumziko, amini leo sikwami.
LEO NIACHE JIKO, MPENZI NIKUPIKIE
Leo nimedhamiria, kulitumikia jiko.
Pia ninakupokea, kwenye hii ada yako.
Lakini uonje pia, mapishi ya mume wako.
LEO NIACHIE JIKO, MPENZI NIKUPIKIE
Nitakupikia ndizi, nachanganya na mihogo.
Naongeza na viazi, naweka boga kidogo.
Kisha naunga na nazi, bokoboko mkorogo.
LEO NIACHIE JIKO, MPENZI NIKUPIKIE.
Pia nazitengeneza, chapati nzuri za maji.
Laini za kutoweza, kwa marage ama uji.
Juu yai naongeza, nogesho kwenye ulaji.
LEO NIACHIE JIKO,MPENZI NIKUPIKIE.
Githeri ama mayai, kama unapendelea.
Maziwa ama ni chai, mwenyewe utachagua.
Chungwa ndizi na papai, taweka kwenye sinia.
LEO NIACHIE JIKO,MPENZI NIKUPIKIE.
Wanaume tunajua, kupika kuliko wake.
Na kama haukujua, ndo leo ifahamike.
Usije kujisumbua, mashindano uumbuke.
LEO NIACHIE JIKO,MPENZI NIKUPIKIE.